Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo likiwa limefikia siku sita baada ya uchaguzi mkuu uliogubikwa na kashfa za wizi wa kura na kucheleweshwa kusambazwa vifaa vya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi ya DRC – CENI, Denis Kadima amesema hawatosita kufuta baadhi ya matokeo ya uchaguzi iwapo udanganyifu utathibitishwa.
Amesema, vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi hazikupangwa na CENI na amewatupia lawama baadhi ya wanasiasa ambao walijaribu kuiba kura kwa kushirikana na baadhi ya mawakala wa tume ya uchaguzi.
Hadi jana Desemba 25, 2023 baadhi ya maeneo yaliendelea kupiga kura, ikiwa ni siku tano baada ya uchaguzi kufanyika huku hatua hiyo ikilenga kuwapa fursa wapiga kura wote ambao vifaa vya uchaguzi vilichelewa kufikishwa kwenye maeneo yao Desemba 20, 2023.
Hadi kufikia sasa, CENI imetangaza matokeo ya kura milioni 1.9, kati ya jumla ya wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha na rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kwenye matokeo hayo ya awali.