Mitandao mbalimbali ya kijamii, imekuwa ikiripoti kwamba mtu tajiri zaidi duniani na mwanzilishi wa SpaceX, Elon Musk anatazamiwa kuzindua uwekezaji wake wa hivi karibuni wa hoteli huko katika Sayari ya Mars.
Taarifa hizo, zimekuwa zikiambatana na baadhi ya picha za hoteli hiyo yenye mandhari nzuri na inayodaiwa kuwa, usiku mmoja wa malazi utamgharimu mteja kiasi cha dola milioni 5, bila kufafanua uhalisia wa maisha ya huko kijiografia na maisha halisi.
Uthibitisho.
Mtu mmoja Mfaransa, asubuhi ya Julai 27, 2022 alitweet kupitia mpini wa @mcphils_ alitweet kuwa nanukuu, “Hoteli ya Kwanza huko Mars na Elon Musk inatazamiwa kufunguliwa hivi karibuni kwa $ 5 Milioni kwa usiku.” Tweet ambayo ilipata zaidi ya retweets 5,000 na likes 18,000 kwa wakati huo.
Chapisho hilo pia lilisambazwa sana kwenye Facebook na African Report Files, Rockreal TV, na mitandao mingine ya kijamii ikiwemo Blogu za mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya na hapa kwetu Tanzania pia kuna baadhi ya Blogu na kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii za mtu mmoja mmoja zilichapiasha habari hii.
Dai la awali la Musk.
Mwaka 2020, Musk alikuwa amedai kuwa SpaceX itawapeleka watu milioni moja kwenye sayari ya Mars ifikapo 2050. Hesabu za Mask zilitegemea kuwa na chombo kinachoitwa Starship ya kuendesha takriban safari tatu kwa siku na kwa hivyo kuwa na takriban safari 1,000 kwa mwaka.
Awali Musk alikuwa ameelezea mipango ya kufika Mars wa Mars Base Alpha ambapo pia alizungumzia kuhusu mradi huu na maelezo machache yanayokusudiwa lakini picha zilizotolewa na Musk 2018, zilionesha tovuti za kutua kwa roketi ya Falcon Heavy na miundombinu yake jinsi itakavyoendeshwa na shamba kubwa la kuzalisha mionzi ya jua.
Kuhusu Mars.
Kulingana na Wanasayansi wa Mamlaka ya Taifa ya Hali ya Hewa na Anga Nchini Marekani – NASA, wanasema Mars ni sayari ya nne kutoka kwenye Jua na huko kuna vumbi, baridi, jangwa na anga nyembamba. Ni sayari inayobadilika-badilika kimisimu, ikiwa na sehemu za barafu, makorongo, volkeno mfu na utulivu usiotabirika.
Walidai Mars ni mojawapo ya sayari iliyochunguzwa zaidi katika mfumo wa jua, na ndiyo sayari pekee ambayo Vyombo mbalimbali vya anga vimetumwa kuzurura katika mazingira ya kigeni ili kufanya udadisi wa mambo, ikiwa na eneo la maili 2,106 (kilomita 3,390), Mars ni karibu nusu ya ukubwa wa Dunia.
Kutoka umbali wa wastani wa maili milioni 142 (kilomita milioni 228), Mars iko umbali wa vitengo 1.5 vya angani kutoka kwenye jua. Kitengo kimoja cha astronomia (kifupi kama AU), ni umbali kutoka Jua hadi Dunia na umbali huu huchukua mwanga wa jua dakika 13 kusafiri kutoka kwenye Jua hadi Mars.
Mars ni nyumba ya volkano kubwa zaidi katika mfumo wa jua, ikiwa na eneo lenye kina kirefu mara tatu zaidi ya Mlima Everest wa Duniani wenye msingi wa ukubwa wa jimbo kama la New Mexico.
Utafiti wa kutosha ulifanywa kwenye sayari ya Mars na ndege za Viking, rova za Spirit na Opportunity, Phoenix lander na Curiosity rover huku ushahidi ukionesha kwamba sayari hiyo ilikuwa na viumbe wengi zaidi kuliko ilivyo leo, lakini ikiwa viumbe hai viliwahi kuwepo huko, hilo bado haijulikani.
Uchunguzi.
Vyombo vingi vya angani visivyo na wafanyakazi, vilitumwa kwenda Sayari ya Mars na Taifa la Marekani, Muungano wa Sovieti, Ulaya, India, Falme za Kiarabu, na Chinaili kuchunguza uso wa sayari hiyo, hali ya hewa na jiolojia.
Na hadi kufikia leo, Mars ni imetembelewa na vyombo 14 vya anga vinavyofanya kazi, nane viko kwenye obiti: 2001 Mars Odyssey, Mars Express, Mars Reconnaissance Orbiter, MAVEN, Mars Orbiter Mission, ExoMars Trace Gas Orbiter, Hope Orbiter, na Tianwen-1 Orbiter.
Nyingine sita ziko juu ya uso: lander ya InSight, Mars Science Laboratory Curiosity rover, rover ya Perseverance, helikopta ya Ingenuity, lander ya Tianwen-1, na rover ya Zhurong.
Hata hivyo, misheni ya Rosalind Franklin rover, iliyoundwa kutafuta ushahidi wa maisha ya zamani, ilikusudiwa kuzinduliwa mwaka 2018 lakini imecheleweshwa mara kwa mara na tarehe ya uzinduzi ilisogezwa hadi 2024, ambapo dhana ya sasa ya misheni ya kurejesha sampuli ya Mars ingezinduliwa mwaka 2026 na NASA na ESA.
Mipango kadhaa ya misheni ya wanadamu kwenda Mars imependekezwa katika karne zote za 20 na 21, lakini hakuna iliyofanikiwa. Sheria ya Uidhinishaji wa NASA ya 2017 ilielekeza kuchunguza uwezekano wa ujumbe wa wafanyakazi wa Mars mapema miaka ya 2030, ripoti iliyotokana hatimaye ilihitimisha kuwa hii haitawezekana na mwaka 2021, Uchina ilikuwa inapanga kutuma misheni ya wafanyakazi wa Mars mnamo 2033.
Ukweli kuhusu Hoteli / Hitimisho.
Ushahidi uliopo, unathibitisha kwamba machapisho na ripoti zinazodai kwamba Elon Musk hivi karibuni atafungua hoteli huko Mars kwa dola milioni 5 kwa usiku ni za uongo na za kupotosha. Hadi kufikia sasa hakuna uthibitisho wa maisha kwenye sayari hiyo nyekundu, inayojulikana kama Mars na Musk pia hakutoa madai kama hayo katika siku za hivi karibuni.
Uhakiki huu wa ukweli wa kufanikisha makala haya ulifanywa kwa msaada na ushirikiano na Kituo cha Demokrasia na Maendeleo (CDD).