Ole Gunnar Solskjaer yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha dili lake la kurejea kwenye kazi yake ya ukocha baada ya mkali huyo wa zamani wa Manchester United kupewa nafasi kubwa ya kutua Besiktas.
Miamba hiyo ya Super Lig ya huko Uturiki ipo sokoni kusaka kocha wa tatu msimu huu kufuatia Riza Calimbay kufutwa kazi baada ya mechi saba tu za kuinoa timu hiyo.
Na kwa mujibu wa ripoti za kutoka Uturuki, Solskjaer ndiye anayepewa nafasi baada ya kufanya mazungumzo na klabu hiyo.
Besiktas anashika namba tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Uturuki, lakini ipo nyuma kwa pointi 17 dhidi ya vinara, Fenerbahce.
Mabosi wa timu hiyo hawafurahii namna timu inavyocheza kwenye mbio za ubingwa wa ndani na vita ya kusaka tiketi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Solskjaer, 50, amekuwa hana kazi tangu alipofukuzwa Man United katikati ya msimu wa 2021/22.
Alinoa klabu hiyo ya Old Trafford kwa misimu mitatu, ambapo awali alikuwa kocha wa muda alipokabidhiwa mikoba ya Mreno Jose Mourinho.
Katika kipindi chake, raia huyo wa Norway aliisaidia Man United kufika fainali ya Europa League na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, Solskjaer alikutana na pingamizi nyingi kwamba Man United ilimpa kazi kwa kuwa tu alikuwa mchezaji wao wa zamani na si kwa sababu ya uwezo wake.
Alifutwa kazi baada ya timu yake kuruhusu mabao 15 katika mechi tano za Ligi Kuu England, ikiwamo kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Liverpool.
Kama atatua Besiktas, basiatakwenda kukutana tena na beki wake wa zamani, Eric Bailly.