Mahakama ya Wilaya ya Babati, imeifuta kesi ya ukatili iliyokuwa inamkabili Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul ya tuhuma za unyanyasaji wa kijana Hashim Ally iliyokuwa ikimkabili.
Uamuzi huo, umetolewa hii leo Desemba 27, 2023 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Babati, Victor Kimario na kusema uamuzi huo unatokana na wasilisho la Mkurugenzi wa Mashtaka – DPP, la kudai hana nia ya kuendelea nayo.
Kesi hiyo, ilifunguliwa na wakili Peter Madeleka chini ya kifungu cha 128 (2) na (4) cha Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA), kama ambavyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hata hivyo, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Madeleka umesema haujakubaliana na maamuzi hayo ya Mahakama na kwamba wanatarajia kukata rufaa.