Umoja wa Mabalozi wa nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania wamekabidhi msaada wa mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba kwa wananchi waliokumbwa na mafuruko na maporomoko ya udongo katika eneo la Katesh Wilayani Hanang mkoa wa Manyara.
Akikabidhi msaada huo kwa Serikali, Kiongozi wa Mabalozi hao na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed amesema kundi la Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao Tanzania lina mabalozi 24 ambao wameonesha kuguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kuona ni vyema kuwasaidia wananchi hao pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji.
Amesema umoja wa Mabalozi wa Afrika nchini wameguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kwa umoja wao wamechangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo la Katesh ili kurejesha makazi ya wananchi hao.
“Tunaendelea kuomba Mungu awajalie subira na kwa wale waliopoteza maisha wapumzike kwa amani. Kadhalika, kwa waliosalia basi msaada huo utawasaidia kujenga makazi yao na kuendelea na maisha kama ilivyokuwa awali,” alisema Dkt. El Badaoui Mohamed
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Serikali amewashukuru mabalozi hao kwa umoja wao na kwa msaada huo ambao utasaidia kurejesha makazi ya wananchi wa Katesh.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa baada ya kupokelewa utaratibu utafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa ili mifuko hiyo iwasilishwe katika Kijiji cha Katesh, Wilayani Hanang.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu, baada ya kutokea kwa maafa yale sote tunajua Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha maisha ya watu yanarejea katika hali ya kawaida. Msaada huu utasaidia katika ujezi wa nyumba zilizoathiriwa na mafuriko hayo,” alisema Mhe. Balozi Mbarouk.
Balozi Mbaorouk amesema msaada huo ni uthibitisho kwamba uhusiano kati ya Balozi zote zilizopo nchini hususan Balozi za Afrika ni mzuri na kwa msaada huo wameonesha ushirikiano mkubwa na Serikali ya Tanzania.
Tarehe 02 Disemba 2023 eneo la Katesh, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, lilikumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha vifo vya watu 89, kujeruhi wakazi wa eneo hilo na kuharibu makazi na mazao yao.
Msaada huo walioukabidhi kwa Serikali ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa, tarehe 7 Disemba 2023, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba alipokutana na Jumuiya ya wana diplomasia nchini ili kuwapa taarifa rasmi ya Serikali juu ya tukio hilo na hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya kutokea kwa maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Mkoani Manyara tarehe 02 Disemba, 2023.