Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Leonce Rwegasila amewataka waendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda, kuanza kusajili vijiwe vyao ili vitambulike na viongozi kwa lengo la kuziba mianya ya wahalifu wanaojipandikiza kwao.
Kamishna Rwegasila aliyasema hayo wakati alipokuwa akitoa elimu kwenye vijiwe vya bodaboda katika Kata za Dumila, Kitete, Msowelo Rudewa na Kasiki Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, iliyowalenga vijana wanaofanya shughuli za bodaboda kwa kuwatahadharisha juu ya matukio ya wizi, kushambuliwa na wahalifu unaowasababishia ulemavu wa kudumu hata vifo.
Alisema, “tamaa ndio imekuwa chanzo kikubwa cha uhalifu kutokea bodaboda wamekuwa wakitamanishwa kwa kulipwa kiasi cha pesa nyingi kwa safari fupi bila kushtuka kuwa anaingia kwenye mtego wa wahalifu.”
“Ukimuona abiria anakupa elfu 10 kwenye safari ya elfu 2, pokea hiyo hela gawana na mwenzako mwende pamoja na ukiona abiria huyo anakataa fahamu ya kuwa sio mtu mzuri mtolee taarifa Polisi,” alisema.
Aidha, aliwataka pia kuchukua tahadhari ya wateja wanaowapakia hasa ambao ni wageni kwenye mazingira yao, kuacha tamaa ya pesa na kujali maisha yao na kuhakikisha wanaaga pale wanapoondoka kijiweni.
Amesema, lengo la kuaga ni muhimu ili tukio likitokea papatikane pakuanzia, na wajitahidi kuzingatia sheria za usalama barabarani, kununua pikipiki za halali katika maduka yanayotambulika na kama ni kuuziana basi iwe katika ofisi za serikali.