Mabingwa wa Soka nchini Hispania FC Barcelona wamepania kumsajili Mason Greenwood na wamewatuma maskauti wao watatu wakamuangalie kwenye mechi tatu za mwisho za La Liga alizocheza.
Wawakilishi wa FC Barcelona wakawasiliana na mabosi wa Manchester United kwa ajili ya kuzungumza kuhusu uwezekano wa kumsajili fowadi huyo anayekipiga Getafe kwa mkopo.
Chanzo cha habari kimeripoti: “FC Barcelona inavutiwa na Greenwood na imepania kumsajili. Kwa sasa ndio timu inayoongoza katika mbio za kuwania saini yake.”
Uhamisho wa Greenwood kwenda FC Barcelona itakuwa jambo kubwa kwake kwani aliambiwa na Man United kwamba hataichezea klabu yake ya utotoni tena.
Mapema mwaka huu, Gazeti la Sun liliambiwa kwamba, Greenwood ameonyesha nia ya kubaki Hispania na kuendelea na maisha yake ya soka baada ya kuondoka Man United.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 22, ameonyesha kiwango kizuri alipotua Getafe mwanzo wa msimu huU na ameendelea kuonyesha makali yake La Liga.
Aidha kwa mujibu wa ripoti Getafe inapanga kumsajili Greenwood pindi mkopo utakapomalizika na itakuwa tayari kutoa Pauni 43 milioni.
Hata hivyo, Man United haijaonyesha ushirikiano kama ipo tayari kumuuza mchezaji wao aliyekulia kwenye kituo cha kukUza vipaji Old Trafford.