Wakati wakitarajiwa kuondoka kesho Jumapili (Desemba 31) kuelekea visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi Cup, Wekundu wa Msimbazi ‘Simba SC’ wamesema wanataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya uzinduzi wa uwanja wa Amaan.
Michuano ya mwaka huu ya Mapinduzi Cup iliyoanza juzi Alhamis (Desemba 28) inafanyika kwenye uwanja wa Amaan ambao umefanyiwa maboresho makubwa na kuzinduliwa juma hili na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema malengo ya klabu na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha ni kutwaa ubingwa huo, kwa sababu utakuwa ni wa kwanza baada ya kukarabatiwa uwanja mpya wa Amaan.
Ahmed amesema wamekaa na Kocha Mkuu na kumwambia umuhimu wa kuchukua kombe hilo, kwani utaendelea kuweka rekodi ya klabu hiyo kutwaa mara nyingi kombe hilo tangu kuanzishwa kwake.
Mnyama atang’oa nanga Kesho Jumapili (Desemba 31) kuelekea Zanzibar kuanza kampeni yetu ya kutafuta ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ndani ya uwanja mpya wa Amaan, wachezaji wote ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa, watakuwa Unguja kwa ajili ya michuano hii.
“Unajua kwa ukubwa wa Simba SC ni lazima tukaweke rekodi katika uwanja mpya, Uwanja wa Amaan umeboreshwa na kuwa wa kisasa zaidi, na sisi Simba SC tunataka kuwa klabu ya kwanza kutwaa Ubingwa ndani ya Uwanja mpya wa Amaan,” amesema Ahmed.
Amesema kikosi cha timu hiyo kipo imara na tayari kwa ajili ya michezo hiyo, huku kocha wao Benchikha akipanga pia kutumia michuano hiyo kuijenga zaidi timu yake kabla ya kurejea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi kusaka tiketi ya kutinga Robo Fainali.
Simba SC inatarajiwa kushuka uwanjani keshokutwa Jumatatu (Januari Mosi) kucheza dhidi ya Maafande wa Kujenga Uchumi (JKU) katika mechi yao ya kwanza ya Kundi B ya michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.
Simba SC iko kwenye Kundi hilo pamoja na timu ya Singida Fountaine Gate, JKU na APR ya Rwanda.
Tayari mchezo mmoja wa kundi hilo umeshachezwa jana Ijumaa (Desemba 29), ambapo Singida FG waliifunga JKU mabao 4-1.