Hofu iliyokuwa imetanda kwa Mashabiki wa Tabora United ya kukimbiwa na kocha wa timu hiyo, Goran Kopunovic, imefifishwa baada ya kocha huyo kutoka Ulaya ya Mashariki kuamua kusalia kwenye kikosi hicho akizima uvumi wa kutaka kutimka kwa madai ya kutolipwa mishahara wa miezi miwili.

Mbali na uvumi wa Goran kutaka kusepa kwa ishu ya mshahara, pia ilidaiwa alikuwa na ofa tatu mezani zilizomchanganya, lakini habari kutoka klabuni hapo zinasema kocha huyo amegeuza mpango baada ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo.

Tabora United iliyopanda daraja na kuanza kuchezea Ligi Kuu msimu huu 2023/24, haijawahi kubadilisha kocha, huku ilkishika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 15.

Goran amesema ameamua kuzikacha ofa zote kutokana na malengo makubwa waliyonayo wachezaji na uongozi kwa ujumla pamoja na upendo wa dhati alionao kwa timu hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa nje na malengo, kwake haikuwa rahisi kuanza kufundisha timu nyingine, kwani kila kitu huwa kinaanza upya na kuchukua muda mrefu kutambua uwezo wa kila mchezaji na namna ya kupanga kikosi.

“Kwa sasa nimeona nibaki na akili moja, hapa Tabora United tuna mradi wa kuufanikisha pamoja, lakini sitaacha kuzishukuru klabu zote zilizotaka kunipa kazi ila naona bado nina deni hapa,” amesema Goran ambaye ni kocha wa zamani wa Simba SC

“Nimefikiria kama nitaondoka sasa nitawavunja nguvu wachezaji wangu na mashabiki wa Tabora United, pia huko nitakapokwenda nitahitaji muda kujenga uimara kama ambavyo tulijenga hapa Tabora, ni vyema uamuzi huu kuufanya mwisho wa msimu kama nitaona kuna ulazima wa kufanya hivyo” amesema kocha huyo

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 31, 2023
Hugo Loris kucheza soka MLS