Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini, Zanzibar (TAMWA – ZNZ), Dkt. Mzuri Issa amesema jamii inahitaji kutafuta mbinu za kupambana na vitendo vya udhalilishaji ambavyo
vinaripotiwa kuongezeka kiasi cha kuwa na matukio zaidi ya 150 kwa mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa Taarifa aliyoitoa kwa Vyombo vya Habari hii leo Desemba 31, 3023 imeeleza kuwa ripoti ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, inaonesha kuwa ndani ya Oktoba, matukio yalikuwa ni 199 na mwezi Novemba 2023 jumla ya matukio 172 yaliripotiwa.
“Katika matukio hayo, waathirika wakubwa wa vitendo hivyo walikuwa ni wanawake na watoto ikilinganishwa na idadi ya matukio ya mwaka 2022 ambapo jumla ya matukio 1,361 yaliripotiwa, idadi hiyo inaweza kuongezeka kupita kiasi kutokana na idadi kubwa inayoripotiwa kwa kila mwezi ndani ya mwaka 2023,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, TAMWA ZNZ imeeleza kuwa ongezeko hili linahitaji kuangaliwa katika pande kuu mbili ambazo ni vyombo vya kisheria pamoja na jamii kwamba ni kwa kiasi gani sehemu hizo zinachukua jukumu lake ipasavyo.
Taarifa hiyo imetoa mfano kuwa upande wa vyombo vya sheria vinatakiwa vihakikishe haki inapatikana kwa watu wote kama inavyostahiki na kwamba wahalifu wote bila ya ubaguzi walipie makosa yao na kwamba sheria zinahitaji ziwe vizuri, zinatekelezeka ipasavyo na kwamba Maafisa wa vyombo vya sheria wanashughulikiwa ipasavyo pale wanapokengeuka majukumu yao.
“Jamii kwa upande wake inapaswa kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kutoa elimu kwa watu walioko katika makundi hatarishi ili wasifanye vitendo vya kudhalilisha wengine, kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji na kutoa ushahidi pale inapohitajika,” ilifafanua zaidi taarifa hiyo.
Hata hivyo, TAMWA ZNZ inasema kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mtakwimu kwa mwezi wa Novemba kati ya matukio 172 ni tukio moja pekee ndilo lililofikishwa Mahakamani, hali ambayo inahitaji kuangaliwa vizuri.
“Changamoto nyengine ni juu ya ukosefu wa utumiaji mzuri wa sheria kwa mfano sheria ya ushahidi No. 9 ya mwaka 2016 imetoa fursa ya kutumia ushahidi wa kielektroniki lakini bado hautumiki ipaswavyo na hivyo kuhatarisha kupotea kwa mafaili na kuleta usumbufu kwa watoa ushahidi hasa watoto na watu wenye ulemavu,” ilieleza.
Aidha, TAMWA ZNZ imetoa wito kwa vyombo vya sheria kuzidisha kasi ya upelelelezi na kuwekeza katika teknolojia kwa ajili ya kusikiliza malalamiko na kuwapa unafuuu watoto wadogo, pia ikidai inaendelea kutoa wito kwa vijana kujipangia mipango madhubuti ya kutokuingia katika vitendo hivyo ikiwemo kuacha kufuata vishawishi, kutokuendekeza
mihemuko na pia kujidhibiti dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.