Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Angel Gamondi amemtaka mchezaji mpya wa timu hiyo, Augustine Okrah kuonesha kwa vitendo uwezo wake ili kudhihirisha imani waliyonayo viongozi na mashabiki wa timu hiyo juu yake.

Okrah aliyeitumikia Simba SC msimu uliopita, amejiunga na Young Africans kwenye dirisha dogo msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea timu ya Bencham United ya nchini kwao Ghana.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema timu yake ilihitaji mchezaji wa kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kulingana na ugumu wa mashindano wanayoshiriki na ukubwa wa Young Africans, hivyo anapaswa kujituma na kuonesha kwa vitendo kwamba anastahili kucheza timu hiyo.

“Sihitaji kuzungumza mambo mengi kuhusu yeye kama kocha nitampa nafasi aonyeshe kwa vitendo ubora wake utakaompa nafasi ya kucheza zaidi, endapo atashindwa kufanya kile tunachokitarajia kutoka kwake atawapisha wengine wacheze,” amesema Gamondi.

Kocha huyo amesema kwa viwango na malengo ya Young Africans, hivi sasa hawahitaji kumpa muda mchezaji kulingana na aina ya mashindano lakini pia uhitaji wa matokeo kuwa mkubwa katika kila mechi.

Amesema kwenye kikosi chake anao wachezaji wenye uwezo na rekodi nzuri huko walikotoka, lakini wameshindwa kukopi mapema wakiwa Yanga na yeye ameshindwa kuwatumia sababu ya uhitaji wa matokeo.

Malengo ya Young Africans msimu huu ni kufika Robo Fainali kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kutetea mataji yote ya ndani ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Madereva wahimizwa uhakiki wa Magari ya Wanafunzi
Kocha Azam FC amwagia sifa Navarro