Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Mecky Maxime amewaahidi mabosi wa timu hiyo mambo makubwa kutokana na mifumo ya kisasa anayoipandikiza kwa wachezaji wake.

Kocha huyo amesema timu hiyo ina wachezaji wazuri isipokuwa kilichokuwa kinawasumbua wasipate matokeo mazuri ni mfululizo wa vipigo.

“Kufungwa mfululizo kumevuruga saikolojia ya wachezaji, baada ya kukabidhiwa timu kitu cha kwanza nilichoanza nacho ni kujenga saikolojia zao na kupandisha ari ya upambanaji ili waweze kufanya vizuri,” amesema Maxime.

Kocha huyo amesema mipango yake ni kuiondoa Ihefu FC nafasi za mkiani waliyopo hivi sasa na kuipandisha nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.

Amesema anatambua ugumu uliopo kwenye ligi ya msimu huu lakini anajivunia uwezo wa wachezaji wake pamoja na wasaidizi wake, hivyo hakuna kitu kitashindikana.

Ihefu FC ambayo hadi sasa imeshatimua makocha wawili ambao ni Zuberi Katwila na Moses Basena, ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 13 katika michezo 14.

Utata kauli ya Ruto: Jaji Mkuu, Odinga wamkosoa hadharani
TAHOA yazigusa familia za waathiriwa Hanang'