Klabu ya Simba SC inatajwa kuhamishia rada zake kwa Kiungo kutoka nchini Senegal Babacar Sarr, katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la usajili ambacho rasmi kitafikia tamati Januari 15.
Hadi sasa Simba SC imeshakamilisha usajili wa Saleh Masoud Karabaka, lakini kabla yake ilielezwa imeshampa mkataba winga kutoka Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi na winga wa Tanzania Prisons, Edwin Balua huku ikikamilisha taratibu za mwisho za usajili wa Mshambuliaji nyota kutoka Zimbabwe, Michael Charamba kutoka Chicken Inn.
Kwa sasa Uongozi wa Klabu hiyo ya Simba SC unatajwa kuwa katika hatua za kumsajili Kiungo Mkabaji Babacar Sarr aliyewahi kucheza dhidi ya Cristiano Ronaldo wa Al Nassr katika mechi za michuano ya Klabu Bingwa ya Nchi za Kiarabu iliyopigwa Julai 31, mwaka jana wakati akiichezea US Monastir ya Tunisia iliyocheza na Young Africans msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Katika mechi hiyo, Al Nassr ilishinda mabao 4-1 na ndio iliyobeba taji ikiifunga Al Hilal.
Kiungo huyo mkabaji anayetumia zaidi mguu wa kulia, mwenye umri wa miaka 26 jina lake lipo mezani kwa mabosi wa Simba SC wakimpigia hesabu za kumsajili, lakini wakisubiri uamuzi wa kocha mkuu, Abdelhak Benchikha ambaye naye alikuwa na jina la Eric Mbongossoum ili kuamua nani abebwe kati yao.
Utamu ni kwamba kwa sasa hana timu tangu alipomaliza mkataba na Monastir, Novemba mwishoni mwa mwaka jana, hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kula shavu kama mambo yatakwenda freshi.
Benchikha amewaangiza mabosi wa Simba SC kuletewa kiungo wa chini atakayeweza kufanya kazi nyingi na kuituliza timu baada ya waliopo kama Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma kushindwa kumpa anachotaka licha ya kazi nzuri wanayofanya kikosini kwa sasa.
Mbali na Sarr na Mbongossoum ambaye ni raia wa Chad, mezani kwa mabosi wa Simba SC pia kuna jina la kiungo Mkongo, Mike Miche aliyeongezwa na viongozi kumpa nafasi kocha kuchagua amtakaye.
Habari kutoka ndani ya Simba SC zinasema kuwa uamuzi wa mwisho upo ndani ya saa 48 kuanzia leo Jumamosi (Januari 06) ili kupitishwa kwa jina moja na wale watakaoshindwa kupenya wataachana nao mazima.
Raia huyo wa Senegal mwenye urefu wa mita 1.83 alizaliwa Julai 24, 1997 katika mji wa Thies, Senegal amewahi kukipiga kwenye timu za Wallydann, AS Pikine, Mbour PC na Teungueth zote za Senegal kabla ya kutua Olympique Beja aliyotwaa nayo taji la Kombe la Tunisia msimu uliopita kabla ya kusajiliwa US Monastir aliyoichezea msimu huu kwa nusu msimu mechi saba na kufunga bao moja.
Inaelezwa Kocha Benchikha ametaka kuletewa haraka kiungo wa aina hiyo atakayekuja kutuliza eneo la kiungo mkabaji akichukizwa na hatua ya ukuta wake kuruhusu mabao mara kwa mara.
Bado mabosi wa Simba SC wanapambana kumshawishi Sarr ambaye inaonyesha anahitaji dau kubwa la usajili.
“Tunazungumza naye kama tutakubaliana tutafanya. Uamuzi huu wote tunamshirilisha na kocha (Benchikha) ili tuamue kwa pamoja,” amesema bosi mmoja wa wa juu wa Simba SC.
“Tunatakiwa kusajili kiungo mkabaji haraka. Kuna mambo kocha (Benchikha) hayafurahii kwenye eneo la kiungo mkabaji ndio maana kumekuwa na presha kubwa ya kumpata mtu wa aina hii.”
Simba SC inayoshiriki michuano ya kimataifa kama itampata mchezaji huyo, basi itakuwa imepata dodo kwenye mwarobaini kwani kwa sheria za CAF anaruhusiwa kucheza mashindano hayo.