Namibia imepunguza kikosi chake ambacho kitashiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, hadi kufikia 23 kutoka wachezaji 28 ambao walikuwa wakijiandaa nchini Ghana, Chama cha Soka cha nchi hiyo kilisema juzi.
Waliwasilisha kikosi chao cha mwisho kwenye Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kabla ya Jumatano, ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya kufanya hivyo, huku wachezaji 11 wakirejeshwa kutoka katika kikosi cha Namibia kilichoshiriki AFCON 2019 nchini Misri.
Wachezaji hao ni pamoja na Peter Shalulile, mfungaji wa mabao mengi katika klabu ya Afrika Kusini ya Mamelodi Sundowns na beki Ryan Nyambe, aliyekulia England na kuzichezea Blackbum Rovers na Wigan Athletic kabla ya kutua Derby County msimu huu.
Hii ni mara ya nne kwa Namibia kushiriki fainali hizo za Afrika, ambako hawajawahi kushinda hata mchezo mmoja hadi sasa.
Namibia itaanza kampeni zake ‘AFCON 2023’ kwa kucheza dhidi ya Tunisia, Afrika Kusini na Mali katika mechi zake tatu za Kundi E nchini Ivory Coast, ambazo zinatarajia kuanza wikiendi ijayo.