Klabu ya Arsenal ipo kwenye mazungumzo ya kusitisha mkataba wa mkopo wa winga Marquinhos ili arejee Emirates haraka baada ya kukosa muda wa kucheza huko FC Nantes alikopelekwa.
Staa huyo wa Kibrazili alijiunga na Arsenal wakati wa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2022 akitokea Sao Paulo, lakini baada ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza mabosi wa timu hiyo walimtoa kwa mkopo ili akapate uzoefu.
Baada ya kutumikia nusu ya pili ya msimu uliopita kwa mkopo huko Norwich City, Marquinhos mwenye umri wa miaka 20, alijiunga na Nantes kwa mkopo mwingine Agosti mwaka jana.
Hata hivyo, kwenye timu hiyo ameanzishwa katika mechi moja tu, hivyo klabu yake inafikiria kumrudisha Emirates kwa mujibu wa Gazeti la Ufaransa la L’Equipe.
Kwa ujumla winga huyo kinda amecheza mechi saba tu, kwenye kikosi cha Nantes.
Kiwango cha Marquinhos kimewavutia wengi na kuna nyakati beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown alikuwa akimlinganisha winga huyo na staa Bukayo Saka baada ya kufunga na kuasisti katika mechi yake ya kwanza ya Europa League dhidi ya FC Zurich, Septemba 2022.
Arteta anatambua uwezo wa Marquinhos na ndio maana anataka kumrudisha kwenye timu yake, kwa sababu hapati nafasi ya kutosha ya kucheza.