Wabunge wateule 82 akiwemo Gavana wa jiji la Kinshasa na Mawaziri wa nne wa Serikali ya DRC wamefutwa katika orodha ya wagombea kutokana na kuhusishwa na vitendo vya rushwa, wizi wa kura na kushikilia kinyume cha sheria vifaa vya kielektroniki vya kupigia kura.
Uamuzi huo umechukuliwa na Tume ya uchaguzi Nchini humo – CENI, ambayo pia imesema imefuta matokeo ya uchaguzi wa majimbo mawili kufuatia kupatikana kwa ushahidi wa kukiukwa kwa sheria za uchaguzi.
Msemaji wa CENI, Patricia Nseya amesema wamechukua uamuzi huo baada ya ripoti ya uchunguzi iliyoufanya kuonesha baadhi ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kwenye majimbo hayo walishiriki kufanya vitendo vya udanganyifu.
Hatua hiyo inakuja wakati Mahakama ya Katiba nchini humo ikitarajiwa kusikiliza kesi iliyowasilishwa na mgombea huru wa Urais, Theodore Ngoy ya kupinga uchaguzi huo wa Desemba 20 huku upinzani ukiomba uchaguzi huo urudiwe kutokana na uwepo wa kasoro nyingi na madai ya udanganyifu wa kura.