Beki Raphael Varane anaweza kupewa nafasi ya kubakia Manchester United kwa masharti yaliyopunguzwa anapokaribia mwisho wa mkataba wake unaoelekea ukingoni.
‘Mashetani Wekundu’ hao awali walikataa kuanzisha kipengele chao cha nyongeza cha miezi 12 katika mkataba wa Varane, ambao unatarajiwa kumalizika msimu huu wa majira ya joto, huku kukiwa na wasiwasi juu ya gharama ya mkataba wake wa sasa.
Man United wanataka kuketi na Varane kujadili mkataba mpya ambao ukikubaliwa utamfanya mlinzi huyo wa Ufaransa kulipwa mshahara mdogo.
Vyanzo vimeeleza kuwa, Varane anaweza kufikiria chaguo kama hilo, baada ya kusema wazi kwamba anatarajia kumaliza kazi yake katika moja ya timu tatu ambazo amewakilisha katika maisha yake ya mazuri kisoka.
Varane aliibuka kama nyota wa ujana huko Lens kabla ya kuimarisha kiwango chake kama mmoja wa mabeki bora wa kizazi chake akiwa na Real Madrid.
Madrid kwa sasa hawafikirii kumnunua Varane, huku Kocha Carlo Ancelotti hivi majuzi akithibitisha kuwa hawatamsajili beki mpya wa kati mwezi huu.
Licha ya nia ya Varane kukwepa kujiunga na timu mpya, imeelezwa kuwa maofisa wa Saudi Arabia wako tayari kumpa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ofa msimu wa majira ya joto na wana matumaini kuhusu nafasi yao ya kumshawishi Varane kuhama.
Hadi sasa Varane hajatoa mapendekezo yoyote kwamba atapokea ofa kutoka Saudi Arabia, lakini Mfuko wa Uwekezaji wa Umma, ambao unamiliki vigogo wanne wa nchi hiyo, wanaamini katika uwezo wao wa kuibua maslahi ya mchezaji yeyote.
Kocha Erik ten Hag alithibitisha wakati wa mkutano na waandishi wa habari Alhamisi kwamba United wameanzisha kipengele cha kuongeza mkataba katika mikataba ya Victor Lindelof, Aaron Wan-Bissaka na Hannibal Mejbri, akiongeza kuwa mazungumzo bado yapo kwa Varane na mshambuliaji Anthony Martial, ambaye mkataba wake pia unamalizika msimu huu wa majira ya joto.