Kiungo Jordan Henderson anafikiria kuondoka Saudi Arabia miezi sita pekee baada ya kujiunga na Al Ettifaq kutoka Liverpool kwa mujibu wa ripoti ya Daily Mail.
Kiungo huyo aliondoka Liverpool Julai mwaka huu baada ya miaka 12 pale Anfield, baada ya kusajiliwa na Al Ettifaq inayonolewa na Kocha Steven Gerrard, akiungana tena na mchezaji mwenzake wa zamani wa timu hiyo na England.
Hata hivyo, gazeti la Daily Mail limeripoti Henderson ‘anatamani kurejea katika Ligi Kuu ya England, huku akiwa tayari kukatwa mshahara mkubwa na uwezekano wa kulipa bili ya ushuru ya karibu pauni milioni saba ili kupata uhamisho wa dirisha hili la uhamisho.
Mshahara wake wa pauni 700,000 kwa juma hautozwi ushuru ikiwa atakaa kwa angalau miaka miwili.
Henderson inasemekana kapata ugumu wa kuzoea maisha ya Saudi Arabia, huku hali ya joto ya juu ni sababu zinazochangia kutokuwa na furaha.
Al Ettifaq pia wametatizika kuteka umati mkubwa wa watu msimu huu, ikiwa ni wastani wa mahudhurio ya watu 7,800 pekee licha ya kucheza katika uwanja unaoingiza watu 35,000.
Gerrard naye amekalia kuti kavu baada ya Al Et tifaq kuwa nafasi ya nane kwenye msimamo wa Saudi Pro League, huku msaidizi wake, lan Foster ambaye alisaidia kumshawishi Henderson kuhamia Mashariki ya Kati aliondoka kuchukua kazi ya Kocha wa Plymouth Argyle juma hili.
Ingawa Henderson angependa kujiunga na kikosi cha Ligi Kuu England, ripoti hiyo inaongeza kuwa klabu nyingi za EPL zitakuwa na shida kupata fedha zinazohitajika kukidhi matakwa yake ya mshahara hata kama atapunguza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, amecheza mechi 19 akiwa na Al Ettifaq msimu huu na kutoa asisti tano.