Bondia wa ngumi za kulipwa, Nassib Ramadhani ‘Pacman’ amesema amejipanga kulipiza kisasi dhidi ya mpinzani wake, Emmanuel Naidjala kutoka Namibia.

Ramadhani na Naidjala watacheza pambano sililo la Ubingwa la raundi 10, uzito wa kati litalofanyika Februari 24 mwaka huu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es salaam.

Bondia huyo amesema mwaka 2015 alipigwa kwa pointi na Naidjala akiwa nyumbani kwao Namibia, hivyo awamu hii anajipanga kwa lengo la kupata ushindi na kulipiza kisasi.

“Maandalizi yangu yanaendelea vizuri nashukuru Mungu kwa kupata pambano hilo, ambalo nilihitaji kwa muda mrefu kwa dhumuni la kulipiza kisasi changu kutoka kwa Naidjala,” amesema Ramadhani.

Ramadhani amewaomba Watanzania na wadau wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi katika pambano hili na kuja kushuhudia burudani nzuri kutoka kwake na namna ya urushaji wa makonde.

Promota wa pambano hilo, Abdul Salimu amesema mtanange huo utakuwa na mapambano tisa huku pambano la wanawake likiwa moja ambalo atacheza bondia, Jesca Mfinanga huku mpinzani akiendelea kutafutwa.

“Awamu hii tumeamua kuja na pambano kubwa lenye hadhi la kimataifa ndiyo maana katika mapambano tisa, mapambano manne yatakuwa ya kimataifa ambapo mabondia wa Tanzania watacheza na wapinzani wao kutoka nje ya nchi,” amesema.

Promota huyo amesema pamoja na Ramadhani kucheza pambano la kimataifa lakini bondia Loren Japhet atapanda ulingoni kucheza na Israel Kamwamba kutoka Malawi.

Ramadhani anashuka ulingoni akiwa na kumbukumbu ya kushinda kwa pointi baada ya kumpiga Loren Japhet pambano lilofanyika Julai mwaka jana, jijini Dar es salaam.

Mrithi wa Chama kusajiliwa Simba SC
Hafiz Konkoni aigomea Young Africans