Maafisa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wametoa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali kwa Askari Polisi Mkoa wa Songwe.

Elimu hiyo imetolewa na Elias Mulima ambaye ni Meneja wa Kanda wa ofisi hiyo katika kikao na Maafisa, Wakaguzi na Askari Polisi wa vyeo mbalimbali wa Mkoa wa Songwe na kuzitaja aina za kemikali, madhara yake na jinsi ya kujiokoa endapo ajali itatokea.

Alisema, ni vyema kufahamu athari zitokanazo na kemikali mnazozisindikiza kutoka eneo moja kwenda eneo jengine kwa lengo la kuzuia madhila yatokanayo na kemikali hizo na kwa kufanya hivyo mtajiweka salama katika shughuli za usindikizaji wa kemikali hizo.

Kwa upande wake, Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Gallas Hyera aliwashukuru maafisa hao kwa elimu waliyoitoa na kuwataka Askari mkoani humo kufuata kanuni na taratibu pindi wasindikizapo kemikali hizo ili kujiepusha na madhara ambayo yanaweza kuepukika.

Songwe ni miongoni mwa Mikoa inayopakana upande jirani na nchi za SADC, ambapo usafirishaji wa kemikali kutoka Nchini kwenda  nje kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kama uchimbaji wa madini na ulipuaji wa miamba hufanyika.

Mitandao ya Kijamii chanzo Waziri kubwaga manyanga
Nzwalile amkaribisha Makonda Babati, akemea wapiga dili