Katika harakati za kuhakikisha inaboresha eneo la ushambuliaji, ripoti zinaeleza kwamba mabosi wa Chelsea wanaangalia uwezekano wa kumsajili Mshambuliaji wa Al Itihad ya Saudi Arabia, Karim Benzema ambaye hivi karibuni amekuwa katika sintofahamu na benchi la ufundi la timu hiyo.
Benzema ameachwa kwenye kikosi cha Itihad ambacho kinakwenda kujiandaa na msimu mpya ikiwa ni baada ya kuchelewa kuripoti kujiunga na timu kwa zaidi ya siku mbili.
Hadi sasa hakuna taarifa kamili kutoka kwa mabosi wa timu yake ikiwa wataachana naye au wataendelea, lakini sintofahamu hiyo ndio inawaaminisha Chelsea kwamba huenda wakampata.
Kwa mujibu wa tovuti ya Goal, mbali ya Benzema, Chelsea pia inaangalia uwezekano wa kuipata huduma ya mshambuliaji wa Al Ahli, Roberto Firmino anayedaiwa kuwa hana furaha kwenye timu hiyo.
Wachezaji hao ambao wote walitua Saudi Arabia katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, usajili wao ulitikisa nchini humo na duniani kutokana na umaarufu walionao.