Serikali Nchini, imeamua kwa dhati kuwekeza katika miradi ya Nishati ikilenga kuhakikisha kuwa upatikanaji umeme unakuwa mkubwa kuliko mahitaji ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko hii leo Januari 18, 2024 jijini Dodoma, wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji umeme nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Amesema, “moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ni Sekta hii ya Nishati na ndio maana fedha zimekuwa zikitolewa za kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao gharama yake ni shilingi Trilioni 6.5 na mpaka sasa Serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi Trilioni 5.7 ambayo ni sawa na asilimia 88.7.”

Kuhusu usimamizi wa mradi wa JNHPP, Dkt. Biteko amesema Serikali ipo makini katika usimamizi wake na kwamba kuna mamlaka mbalimbali zinazosimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ufanisi akitolea mfano Timu Maalum ya Wataalam iliyoundwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia mradi huo ambayo inaongozwa na Prof. Idris Kikula.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alieleza Kamati kuwa, mradi wa umeme wa JNHPP kwa sasa umefikia asilimia 95.8 na kwamba mtambo namba Tisa utakaozalisha megawati 235 umeshakamilika na mtambo Namba 8 na namba 7 iko mbioni kukamilika.

Akizungumzia hali ya umeme nchini, Mhandisi Nyamo-Hanga amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazoedelea kufanywa na Serikali ili kupunguza changamoto ya umeme nchini, hali ya upungufu wa umeme itaisha mara baada ya kuwashwa kwa kwa mashine mbili za JNHPP zenye uwezo wa megawati 470 ambazo zinatarajiwa kuwashwa kabla ya mwezi Machi, 2024.

 

Okocha: Nigeria tuna nafasi kubwa AFCON 2023
Maendeleo yanahitaji Viongozi wenye maono - Othman