Maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na ule wa Uraisi mwaka kesho 2025 yamewafanya baadhi ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi – CCM, kuelezea hisia zao za kutaka fomu ya mgombea Uraisi iwe moja, wakidai hakuna kipingamizi katika machaguo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Dar24 Media leo Bungeni Jijini Dodoma Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi wamesema wana imani kubwa na Viongozi wa CCM katika kuelekea kwenye chaguzi hizo.
“Nina imani kutokana pia na uteuzi ambao ameufanya Dkt. Samia kwa kutuletea Mtu bora katika chama chetu cha CCM, Dkt. Nchimbi ni mzoefu sana katika chama, hivyo tuna imani naye kubwa mpaka pale tutakapoelekea kwenye uchaguzi wa Uraisi 2025,” amesema Mbunge wa Lupa, Kasaka.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia, Kamati kuu pamoja na Wajumbe kwa kumpitisha Dkt. Nchimbi kuwa katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM.
“Dkt. Nchimbi anafahamika kama kiongozi ndani ya chama kwa muda mrefu sana na ameanzia mbali,ana uzoefu mkubwa na alishawai kuwa mjumbe wa kamati kuu kwa zaidi ya miaka 14, Mwenyekiti wa umoja wa Vijana miaka 2, Mjumbe wa Halmashauri kuu miaka 19, lakini Mwenyekiti wa Chipukizi CCM,” alisema Prof. Ndakidemi.