Mlinda Lango wa Manchester United, André Onana, huenda akajumuishwa katika kikosi cha Cameroon kwa ajili ya mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya mabingwa watetezi, Senegal itakayochezwa leo baada ya kurejea mazoezini na timu hiyo hapo juzi.
Onana alikosa mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo inayofanyika Ivory Coast baada ya kuruhusiwa kusalia Manchester United na kucheza katika sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur Jumapili iliyopita.
Alisafiri kwa ndege ya kukodi usiku kucha hadi Ivory Coast baada ya mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, lakini alifika saa chache tu kabla ya kuanza kwa mpambano wa Kundi C dhidi ya Guinea, ambapo Cameroon walitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1.
Uamuzi wa kumruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kuacha mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo ilizua utata miongoni mwa mashabiki wa Cameroon.
Katika mahojiano baada ya kuwasili Ivory Coast, Onana aliwaambia waandishi wa habari juu ya mvutano mgumu wa uaminifu kati ya klabu na nchi, haswa kwa wachezaji wa kimataifa kutoka Afrika waliolazimika kuziacha klabu zao za Ulaya kati kati ya msimu ili kushiriki Fainali za AFCON.
“Ni sawa na kuchagua kati ya baba na mama yangu, lakini nchi yangu inatangulia, ndiyo maana nipo hapa,” alisema.