Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), zimepelekea gharama za uletaji wa mafuta nchini (premium) kuendelea kushuka na hivyo kuchangia katika unafuu wa gharama za mafuta ikiwemo ya Dizeli na Petroli.

Dkt. Biteko ameyasema hayo hii leo Januari 19, 2024 jijini Dodoma, wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi Septemba hadi Disemba 2023, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Amesema, “Wizara ya Nishati, EWURA na PBPA, kwa kweli wamefanya kazi kubwa mno ya kushusha gharama za uagizaji mafuta kutoka nje ya nchi, hapo awali gharama hizi zilikuwa zikiongezeka kila mwezi lakini wamesimamia vizuri suala hili na gharama hizi zimeanza kushuka na hivi karibuni mlisikia Waziri wa Kenya akisema bei za mafuta nchini humo zipo juu na za Tanzania zipo chini sababu ya premium, na wengine pia walio nje wanatoa ushuhuda kwamba walau sisi gharama zetu zina unafuu.”

Dkt. Biteko ameeleza kuwa PBPA ambayo inasimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja, ina umuhimu mkubwa nchini kwani ndiyo inayopelekea nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaohitajika, Serikali kufahamu kiwango cha mafuta kinachoingia nchini, kupanga ukusanyaji wa mapato kwa kutumia takwimu sahihi na kupanga bei elekezi ya mafuta.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuiboresha kampuni ya Mafuta ya TANOIL ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC kutokana na umuhimu wake katika biashara ya mafuta nchini na kwamba, TANOIL imekuwa ni kimbilio hasa katika nyakati ambapo zinatokea changamoto za upatikanaji mafuta kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi alieleza kuwa, ili kuboresha mfumo wa upakuaji mafuta melini na kuhakikisha kuwa meli hazikai muda mrefu bandarini, Serikali iliagiza matenki ya TIPER nayo yatumike kupokea na kuhifadhi mafuta na hatua hiyo imewezesha meli za mafuta ya dizeli kutumia siku nne kushusha mafuta badala ya siku tisa na hivyo kuleta unafuu kwa mlaji na kupunguza gharama ambazo Serikali inalipa kutokana na muda wa meli kukaa bandarini.

Amesema kuwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa sehemu maalum ya kupokea na kuhifadhi mafuta ijulikanayo kama single receiving terminal ambapo meli itakuwa na uwezo wa kupakua mafuta kati ya masaa 48 na 36 na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya gharama za meli kukaa bandarini.

Amesema kuwa, kabla ya kuwepo taasisi ya PBPA upotevu wa mafuta kutoka bandarini ulikuwa ni asilimia 0.5 lakini hali ya upotevu kwa sasa imedhibitiwa na upotevu umepungua hadi asilimia 0.1 na kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa upotevu kabisa kwa kufunga mita za kupimia mafuta (flow meter) pamoja na mfumo wa uangalizi wa flow meter (SCADA) ambao utakuwa chini ya PBPA na kwamba mfumo huu utakuwa unafanya kazi muda wote meli ikiwa inashusha mafuta na hivyo kuondoa uwezekano wa upotevu wa mafuta kabisa wakati wa ushushaji wa mafuata.

Ameongeza kuwa, mfumo huo wa SCADA utaweza kuona shughuli ya ushushaji wa mafuta kwa bandari za mikoa inayopokea mafuta ambayo Tanga, Mtwara na Dar es Salaam.

GST kuweka vipaumbele sita utekelezaji wa ajenda Vision 2030
André Onana njia panda AFCON 2023