Licha ya uwepo wa matishio ya kigaidi na itikadi kali, hali ya ulinzi na usalama Nchini ni shwari ambapo Wanamtandao wa kigaidi wamekuwa wakiwalenga Vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35 kisha kuwasafirisha kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi Nchi za Msumbiji, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hayo yamebainishwa hii leo Januari 22, 2024 katika Mkutano wa saba wa CDF na Makamanda Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Jacob Mkunda mbele ya Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema “Hali ya ulinzi na usalama ndani ya Nchi kwa ujumla ni shwari licha ya uwepo wa matishio ya kiusalama hasa tishio la kigaidi na itikadi kali, Wanamtandao wa kigaidi wamekuwa wakiwalingania Vijana wetu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35 kisha kuwasafirisha kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi hususani katika Nchi za DRC, Msumbiji na Somalia hali inayoonesha upo ukuaji wa tatizo hilo hapa nchini.”

Aidha, Jenerali Mkunda ameongeza kuwa Dawa za kulevya, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na ongezekeo la Wahamiaji haramu ni miongoni mwa masuala yanayohatarisha hali ya usalama ndani ya Nchi yetu, hata hivyo matishio hayo yanaendelea kudhibitiwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama.

Mzize, Maxi wakumbuka VIBE la Wananchi
Wakimbizi wameteuliwa nafasi zenye maamuzi - Jenerali Mkunda