Bondia wa ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo, amesema hivi sasa yupo fiti kwa asilimia 98 kumvaa Mbiya Kanku kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Jumamosi (Januari 27).
Mwakinyo atazichapa na Kanku katika pambano la kuwania mkanda wa WBO uzito wa kati, litakalofanyika katika Uwanja wa Amaan Sports Complex, Zanzibar.
Akizungumza Dar es salaam, Mwakinyo amesema bado anaendelea kujifua kuhakikisha anatwaa mkanda huo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Mwakinyo amesema pamoja na kuwa tayari kushinda kwa staili yoyote, lakini lengo lake kubwa ni kumaliza pambano kabla ya raundi ya mwisho.
“Chochote kinaweza kutokea nikiamua kumpiga KO inawezekana, hivyo watanzania watarajie mchezo nzuri kutoka kwangu,” amesema.
Mzawa huyo amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kumshuhudia akionyesha burudani ya aina yake.
Naye Promota wa pambano hilo, Meja Selemani Semunyu amesema muitikio visiwani Zanzibar umekuwa mkubwa kwa a ajili ya pambano hilo.
“Muitikio umekuwa mkubwa sana nawashukuru wadau kwa kutuunga mkono, kutokana na mapokezi haya wananipa hamasa ya kuandaa pambano lingine, “amesema Semunyu.
Mwakinyo atapanda ulingoni akiwa na kúumbukumbu ya kushinda kwa pointi dhidi ya Kuseva Katembo kutoka DRC.