Klabu ya Young Africans ipo tayari kuchukua dau lolote litakalowekwa mezani kwa ajili ya kumalizana na nyota wao raia wa Burkin Faso, Stephane Aziz Ki kama walivyomuachia nyota wao pendwa Fiston Mayele raia wa DR Congo kwenda Pyramids.
Mkataba wa Aziz Ki unatarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu baada ya kuitumikia Young Africans kwa miaka miwili ambapo alijunga nayo Julai 15, 2022.
Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said amesema kuwa, wao wapo tayari muda wowote kupokea ofa ya timu itakayomhitaji Aziz Ki kwani biashara ya mpira ni pamoja na kuuza na kununua wachezaji.
Ameongeza wanatambua kila mchezaji wao kwa sasa ana ofa kubwa hasa kutokana na ubora wa klabu yao, jambo ambalo haliwafanyi kuzikataa ofa hizo mara tu baada ya kukamilika.
“Aziz Ki yupo na ana ofa nyingi kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine wengi, hivyo biashara ya mpira ili ifanikiwe unatakiwa kununua na kuuza kama tulivyofanya kwa Fiston Mayele ambaye kwetu alikuwa ni mchezaji muhimu ila hatukumzuia.
Kuna wachezaji wengi mikataba inaisha mwisho wa msimu huu wengine msimu ujao na yeye (Aziz Ki) pia kuzungumza na timu nyingine sio jambo la ajabu hata sisi tulimpata kwa kuzungumza naye akiwa na timu.
“Kuna ubaya gani kumzuia asiondoke, tumemuachia Mayele. Hivyo tunakaribisha ofa maana ndio biashara ya mpira, Aziz Ki hawezi kucheza hapa milele ipo siku ataondoka tu sio kwake tuni kwa wachezaji wote” amesema Injinia Hersi.