Lydia Mollel – Morogoro.
Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, limeziunganisha familia za Askari na jamii kwa kushiriki kwa pamoja michezo mbalimbali katika kuchagiza siku ya familia ya Polisi (Polisi Family day), wakilenga kuleta umoja na mshikamano baina yao, katika Mapambano dhidi ya Uhalifu.
Akizungumza katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema pia lengo la kukutana kwao ni kufurahi kwa pamoja, kubadilishana uzoefu, kufahamiana na kushirikiana.
Amesema, mbali na kuitumia siku hii kujenga umoja, wanaotumia pia kuwakumbuka Askari ambao wamefariki walifanya shughuli za kipolisi, kuagana na Askari ambao wamestaafu kazi za Jeshi la Polisi pamoja na kukuza ushirikiano na Jeshi la hilo.
Awali, Konstebo wa Polisi Pandu Haji alisema michezo waliyoshiriki inawasaidia katika kuimarisha, kuboresha na kujenga umoja na mshikamano pamoja na kuondoa chuki baina ya familia za kipolisi sambamba na kuondoa hofu ya jamii kwa Jeshi la Polisi.
Amesema ni moja ya tukio bora ambalo limejumuisha watu mbalimbali ikiwemo kushiriki michezo ya kuvuta Kamba, Kukimbiza kuku, kukimbia na magunia pamoja na kucheza muziki.