Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wachezaji, Benchi la Ufundi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kazi kubwa waliyoifanya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Akitoa salamu za Rais Samia Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kupata pointi mbili kwa Stars si jambo dogo, kwani mwaka 2019 Tanzania iliambulia pointi moja tu.
“Mara hii tumesogea mbele tutakapoenda Morocco, tutafanya vizuri zaidi na sisi tunatengeneza timu nzuri na mwaka 2027 tutakapokuwa wenyeji.
“Kwa hiyo tunawapongeza wachezaji lakini tunawaambia kazi inaendelea, tunaenda kujiandaa na mashindano yanayofuata tufanye vizuri mwakani, lakini 2027 tuwe tishio kwa hivyo hongereni wachezaji na poleni kwa safari ndefu lakini mjue serikali iko pamoja na nyinyi,” amesema Msigwa.
Amesema baada ya kutolewa katika michuano ya Ivory Coast, kazi ndio kwanza imeanza ya maandalizi ya michuano inayofuata nchini Morocco mwakani.
Mshambuliaji Simon Msuva amesema wanawashukuru Watanzania kwa sapoti yao waliyowaonesha kwa kuwa bega kwa bega na wao tangu walipoanza hadi walipofika mwisho.
“Tumetolewa lakini wenzetu wanaendelea lakini kikubwa tutajipanga katika mashindano yanayokuja, hatuhitaji tena kuwa wa mwisho naamini kwa uwezo wa Mungu tukiwa wazima tutaendelea kulipambania taifa letu, hilo ndilo kubwa,” amesema Msuva.
Naye Lusajo Mwaikenda amesema kwenye michuano waliyotoka wamepata vitu vikubwa sana kama timu ya taifa na wamejifunza vingi vitakavyowafanya watakaporejea kwenye mashindano yajayo wawe bora zaidi.