Hospitali ya Benjamini Mkapa imeandika historia ya Wagonjwa wa Selimundu kupona, baada ya kupandikizwa uloto miezi michache iliyopita.
Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Januari 30, 2023 Jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Alphonce Chandika amesema awali walitoa taarifa juu ya huduma hiyo ya upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa Selimundu.
“Ni muda mfupi sana tangu tumetoa taarifa ya kupandikiza Uloto kwa Mgonjwa wa Sikoseli, na baada ya hapo tukaanza kupokea wagonjwa hao na mpaka sasa tumetibu watatu ambao wamepona kabisa na wamerejea shule wanaendelea na masomo vuzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa, “hii ni huduma ambayo haijawai kutolewa Nchini isipokuwa hapa Benjamini Mkapa, na tumeona matokeo mazuri, na tukiangalia Tanzania ni Nchi ya nne inayoongoza kwa ugonjwa wa sikoseli, hivyo naamini kupitia huduma hii inayotolewa hapa tunaenda kupunguza ukubwa wa ugonjwa.”
Hata hivyo, Dkt. Chandika amesema huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto kwa Mgonjwa wa Selimundu ni ya msingi, kwani inasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu kwa kuwa na vijana wenye afya njema ya kuweza kufanya kazi
Amewataka pia Wazazi wenye Wagonjwa wa Sikoseli kutowaficha Watoto wao majumbani, kwani huduma hiyo imeletwa kwaajili yao na ugonjwa huo unatibika na unapona kabisa.