Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Morocco ‘ Simba wa Milima ya Atlas’ Walid Regragui amesema kikosi chake hakikucheza kwa kujituma katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora dhidi ya Afrika Kusini usiku wa kuamkia leo, huku akikanusha taarifa za taifa hilo kucheza kwa uwakilishi wa nchi za Kiarabu za Barani Afrika.
Minong’ono iliibuka baada ya mchezo huo kumalizika huku Morocco ikikubali kufungwa 2-0 dhidi ya Afrika Kusini na kutupwa nje ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ ikieleza kuwa Kocha huyo alisema kikosi chake kimeshindwa kuziwakilisha nchi za Kiarabu kwenye michuano hiyo inayoingia kwenye hatua ya Robo Fainali.
Regragui amekanusha uvumi huo alipozungumza na Waandishi wa Habari, akisema huenda baadhi ya watu hawamtakii mema, kwa kushinikiza afungiwe na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kwa kigezo cha ubaguzi.
Akijibu swali kuhusu kuondolewa kwa Misri kutoka kwenye michuano hiyo, na umuhimu wake kama nchi ya Afrika Kaskazini-Kiarabu, Regagui amesema hakupendezwa na hatua ya kutolewa kwa taifa hilo, sambamba na mataifa mengine, na alijibu hivyo kama mdau wa soka.
“Sio jambo ambalo linanivutia… sitajieleza kwa Kiarabu, kwa sababu Kiarabu changu … sitaki kufasiriwa vibaya …, Kila mtu ana njia yake. Ni kweli ni ndugu zetu na tumesikitishwa na kushindwa kwao, lakini pia tuna furaha kwa DR Congo, kuendelea katika michuano hii” amesema.
“Hatuna bendera inayowakilisha au kusema kwamba tunawawakilisha Waarabu hapa. Tulikuja hapa kama Taifa la Morocco sio wawakilishi wan chi za Kiarabu, nah ii ni michuano ya Bara zima la Afrika” ameongeza.
Ushindi wa Afrika Kusini dhidi ya Morocco, umekamilisha idadi ya timu nane zilizotinga hatua ya Robo Fainali ambayo rashi itaanza kuunguruma keshokutwa Ijumaa (Februali 02).
Timu zilizotinga katika hatua hiyo ni Nigeria, Angola, Mali, Afrika Kusini, DR Congo, Guinea, Cape Verde na wenyeji Ivory Coast.