Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi mbalimbali kuongeza kasi mara mbili kuwatumikia wananchi pamoja na kukamilisha ahadi na kuvuka utekelezaji.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika hafla fupi ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri wapya aliowateua hivi karibuni viwanja vya Ikulu Zanzibar hii leo Februari 1, 2024 na kumtaka Waziri wa utalii na mambo ya kale, Mudrick Ramadhan Soraga kuweka juhudi kubwa kupanua wigo katika Sekta ya Utalii hususan utalii wa urithi, mikutano na michezo.
Amesema, Waziri mpya wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, Shaaban Ali Othman anatakiwa kuongeza juhudi katika kuzitatua changamoto za wananchi na kukuza vipato vyao pamoja na fursa za mafuta na gesi katika sekta hiyo, huku akiagiza Wizara ya ardhi kutatua migogoro ya ardhi.
Rais Dkt. Mwinyi pia amesema kujiuzulu kwa Waziri si jambo geni bali ni njia ya uwajibikaji, ameeleza kuwa wakati una wajibika kujiuzulu lazima kuwa mkweli kama kuna sababu za mgongano wa kimaslahi utangaze na kusema wazi sababu zilizokufanya uwajibike.