Serikali Nchini, imesema itaendelea kutenga fedha kupitia vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha inajenga na kukamilisha vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati kote nchini kikiwemo kituo cha Afya Kazuramimba kilichopo mkoani Kigoma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe Nashon Bidyanguze aliyehoji ni lini serikali itakamilisha ahadi ya Sh Milioni 10 alizoahidi Rais wa awamu ya tano katika kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Amesema, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Kazuramimba.
“Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali ilitenga kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri Sh Milioni 158 na kuendeleza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo ujenzi wake upo katika hatua ya ukamilishaji,” alisema Dkt. Dugange.