Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe pamoja na Wakurugenzi wa Wizara ya Afya leo Februari 2, 2024 wmekutana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, wadau wa Hospitali, MSD pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), ambapo wamefanya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Afya Mkoani Dodoma.
Mazungumzo hayo yamelenga kuona ni namna gani Serikali ya Tanzania inaweza kuanzisha ushirikiano wa ununuzi wa dawa adimu moja kwa moja kutoka katika viwanda vya dawa vya nchini Cuba, huku Balozi Polepole akisema hivi sasa Tanzania na ukanda wa nchi za SADC kuna uhaba wa dawa za kutibu magonjwa kama vidonda vitokanavyo na Kisukari, baridi yabisi pamoja na dawa za kutibu ugonjwa wa Vitirigo.
Amesema, “Dawa hizi zinazalishwa nchini Cuba na kiwanda cha Biocube Pharma ambazo zimeonesha matokeo makubwa, hivi sasa wagonjwa wa Kisukari wenye vidonda ambavyo haviponi, nchini Cuba hawakatwi tena viungo kutokana na madhara yanayosababishwa na vidonda hivyo bali hutumia dawa hizo na kupona kabisa.”
Aidha, Balozi Polepole ameongeza kuwa kiwanda hicho kinazalisha dawa za kutibu ugonjwa wa vitirigo (mabaka meupe katika mwili) pamoja na baridi yabisi na imeonekana kuna uhitaji mkubwa wa dawa hizo nchini na ukanda wa nchi za SADC kwani kuna wananchi wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo.
Kwa upande wake, Waziri Ummy amesema “sasa hivi Serikali inatumia gharama kubwa kwa matibabu ya watu wenye vidonda vitokanavyo na Kisukari, Baridi Yabisi pamoja na Vitirigo ambapo takwimu zinaonesha Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee imetumia Shilingi bilioni 1.4 katika matibabu.”