Mshambuliaji mpya wa Simba SC, Freddy Michael Kouablan, amewatoa hofu mashabiki na viongozi wa klabu hiyo kwenye ishu ya kufunga mabao, kwani hiyo ndio kazi yake na hajawahi kukosea katika timu alizotoka.

Raia huyo wa Ivory Coast, ameyesajiliwa na Simba SC hivi karibuni kupitia dirisha dogo akitokea Green Eagles ya Zambia akiwa ameichezea mechi 17 msimu huu na kuifungia mabao 14 na kuasisti mnanne huku katika mechi ya Kombe la ASFC, aliasisti bao la kwanza la Simba SC lililofungwa na Luis Miquissone walipoifumua Tembo FC kwa mabao 4-0.

Akizungumza kabla ya mechi ya leo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, nyota huyo amesema bado anaendelea kuzoea mazingira na maisha mapya ndani ya Simba SC kabla ya kuanza mambo huku akikiri kwa muda mfupi aliokaa amefurahia mambo mengi.

Ameeleza amefarijika sana mapokezi aliyopatiwa na wachezaji wenzake na viongozi bila kuwasahau makocha na wachezaji kwa ujumla. “Kama kuna kitu sina wasiwasi nacho basi ni juu ya ujuzi wangu wa kufunga na kwa namna nilivyoiona timu hakuna kinachoshindikana kupata mabao kutokana na ubora wa wachezaji nilivyouona,” amesema Freddy, huku kocha wa kikosi hicho Abdelhak Benchikha, akisema wachezaji wapya ni mapema kuwapima kwa kutumia mechi moja, akisisitiza bado wana muda wa kufanya vizuri, akiwataka kuzoea haraka mazingira.

“Hatutakuwa na haki kuwapima kwa kuangalia mchezo uliopita ambao tulicheza Dar es salaam na kushinda mabao 4-0, bado ni mapema sana, tuwape muda wanatakiwa kuzoea baadhi ya mambo, lakini wanatakiwa kujituma sana.” amesema Benchikha na kuongeza;

“Changamoto kubwa kwao ni kwamba wamekuja kwenye usajili ambao tayari timu ipo kwenye mashindano na nguvu yao inahitajika pia kubadilisha baadhi ya mambo.”

Mchezaji mkongwe wa kikosi hicho, Shomari Kapombe amewazungumzia wachezaji wapya akisema ni wazuri ila kuna jambo moja hawatakiwi kufanyiwa.

“Wachezaji wapya wameonyesha ubora mkubwa hasa mazoezini, lakini kwa sasa hawatakiwi kuwekewa presha kubwa ya kutakiwa kufanya kazi kwa mafanikio.”

Radi yauwa wawili wakiangalia Luninga
Makala: Mauaji ya Binti kisa Bilauri ya Sharubati