Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi amesema ana matumaini makubwa ya kuifunga Simba SC kutokana na maandalizi waliyofanya kipindi chote ambacho ligi ilisimama.
Geita itaikabili Simba SC Uwanja wa CCM Kirumba, Februari 12 ikiwa ni mchezo wa pili kwa kocha huyo tangu akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi hicho.
Kocha Kitambi amesema anatambua ubora waliokuwa nao Simba SC kuanzia kwenye benchi la ufundi hadi wachezaji, lakini anajivunia uimara wa jeshi lake ambalo linacheza kwa ushirikiano kuanzia kuzuia hadi kushambulia.
“Tunawaheshima Simba SC kwa uzoefu wao lakini hilo halitufanyi kuwaogopa, tumejipanga vizuri kuwakabili na asilimia za kupata ushindi ni kubwa kutokana na maandalizi na maboresho tuliyofanya kwenye kikosi chetu,” amesema Kitambi.
Kocha huyo wa zamani wa Namungo FC, amesema amekuwa akiifuatilia Simba SC katika mechi nyingi walizocheza hivi karibuni na ameona mapungufu yao na amewaelekeza vijana wake ili wayatumie na kupata ushindi pindi watakapokutana.
Geita ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikikusanya pointi 16 katika michezo 13 iliyocheza ya ligi ambapo imeshinda minne, sare minne na imepoteza michezo mitano.