Waziri wa Michezo wa Misri Ashraf Sobhi amewataka Wadau wa Soka nchini humo kumuunga mkono Kocha Mpya wa ‘The Pharaohs’ Hossam Hassan, baada ya kutangazwa na Shirikisho la Soka nchini Misri ‘EFA’ juzi Jumanne (Februari 06).

‘EFA’ ilimtangaza gwiji huyo wa soka nchini Misri kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi, baada ya kumtimuwa Kocha kutoka nchini Ureno Rui Vitória, ambaye alishindwa kufikia malengo ya kuipeleka mbali Misri kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Waziri Ashraf Sobhi amesema ni wakati mzuri kwa kila mdau wa Soka nchini Misri kujihisi furaha kutokana na maamuzi ya ‘EFA’ ambayo yamemuona Kocha Hossam kuwa mtu sahihi wa kuliongoza jahazi la kikosi chao.

Amesema mara kadhaa wadau wa Soka nchini humo walishauri kuteuliwa kwa kocha mzawa, na jina la Hossam lilitajwa mara kwa mara, hivyo anaamini ‘EFA’ imesikia kilio chao na kutenda kwa haraka.

“Kasi ya kufanya maamuzi ni muhimu katika soka na tunawatakia mafanikio wafanyakazi wa Benchi la Ufundi wakiongozwa na Hossam Hassan,”

Egypt

Waziri wa Michezo wa Misri Ashraf Sobhi

“Jukumu letu kama taifa ni kuhakikisha tunamuunga mkono kocha wetu, ili afanye kazi yake kwa usahihi, kwani asilimia kubwa miongoni mwetu tulishauri kuteuliwa kwa kocha mzawa, ‘EFA’ wamefanya hivyo, kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuonesha ushirikiano.”

“Naomba kila mtu amuunge mkono Hossam Hassan ili kwa pamoja tusonge mbele. Ni mmoja wa magwiji wa soka katika nchi yetu ya Misri. Alicheza kwa kujitoa kwa hali yote wakati akiwa mchezaji, ninaamini ari hiyo itaendelea katika kipindi hiki ambacho ni muongoza jahazi letu.” Sobhi aliiambia CBC.

Hossam ataanza na mtihani wa kuhakikisha Misri inafuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026, akitarajia kukabiliana na timu za Burkina Faso Guinea-Bissau, Sierra Leone, Ethiopia na Djibouti huku taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika likiongoza msimamo wa Kundi A kwa kuwa na alama 6.

Kabla ya kutangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Kikosi cha Misri, Hossan alikuwa ametoka kuchukua jukumu la Modern Future siku chache zilizopita, lakini Uongozi wa Klabu hiyo ulikubali kumwachilia.

Hugo Broos: Tulistahili kucheza fainali
Matumizi mifumo ya TEHEMA yaiwezesha OSHA kupata taarifa muhimu