Jitihada za Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), zimezidi kuonekana baada ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na mradi wa kupeleka umeme katika mgodi huo kufikia asilimia 95.
Kituo hicho kinachojengwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.4, kitakuwa na uwezo kupooza umeme wa msongo wa Kilovolt 33 kuwa Kilovolt 11 ndani ya mgodi wa GGML na kina uwezo wa Megawatt 40.
Akitoa taarifa wiki iliyopita mkoani Geita kwa Afisa mkuu wa masuala ya Fedha kutoka AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya GGML, Gillian Doran, Mhandisi mwandamizi anayesimamia ubora na viwango katika miradi ya kampuni hiyo, Maftah Seif alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi Machi kulingana na hali ya upatikanaji wa umeme wa Tanesco.
Alisema kazi kubwa iliyobaki sasa ni kukamilisha ufungaji wa mifumo ya mitambo hiyo pamoja na kuanza majaribio ya mitambo hiyo katika kituo hicho.
Awali akifafanua kuhusu zaidi kuhusu mradi huo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia/ushirika Afrika, Simon Shayo alisema Tanesco hivi karibuni wamekamilisha ujenzi wa laini ya kilovolt 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita huku ujenzi wa laini ya kilomita sita yenye kilovolt 33 kuelekea katika mgodi wa GGML ipo katika hatua za mwisho.
Alisema licha ya kwamba kampuni nyingi za madini tangu miaka ya 2000 hutumia umeme wanaouzalisha wenyewe, sasa Serikali imekuwa na jitihada za makusudi kufungamanisha sekta ya nishati na sekta kubwa za uzalishaji kwa kuzalisha umeme unaotosheleza mahitaji ya wawekezaji wakubwa.
“Sisi kwa sekta ya madini tunaona hii kama ni baraka kubwa kwa sababu huwezi kuendesha migodi mikubwa kama ya kwetu (GGML) kwa kutumia jenereta,” alisema.
Alitoa mfano kuwa GGML hutumia Megawati 40 ambazo huzalisha kwa mafuta ya dizeli lakini sasa wanatamani kuona mradi wa kupeleka umeme wa Tanesco katika mgodi wa kampuni hiyo ukikamilika ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Tukijiunga tu na Tanesco kwenye gridi ya Taifa na kutoka kwenye umeme tunaouzalisha wenyewe, tutapunguza gharama za umeme kwa asilimia 50, tuta-save dola za Marekani milioni 19 kila mwaka. Pia tutapunguza hewa ya ukaa kilotons 81 kufikia 2030,” alisema.
Alisema kwa kuwa nchi ipo katika mipango ya kuwekeza pakubwa katika sekta ya madini kwa kuanzisha migodi ya uzalishaji wa madini mengine sehemu mbalimbali nchini, ni dhahiri kuwa Tanesco itafanikiwa kuongeza mapato makubwa kutokana na mchango wa migodi hiyo kwenye matumizi ya umeme.