Kiungo wa kati wa Chelsea, Enzo Fernandez anatazamiwa kubakia katika klabu hiyo, wakala wa mchezaji huyo amethibitisha huku kukiwa na uvumi kwamba, anafikiria kuondoka Stamford Bridge.

Fernandez alijiunga na Chelsea Januari mwaka jana kwa ada iliyokuwa rekodi ya England kwa Pauni Milioni 108, akihamia London Magharibi kutoka Benfica ndani ya wiki chache baada ya kushinda Kombe la Dunia la 2022 akiwa na Argentina na kusaini mkataba wa miaka nane na nusu hadi msimu wa joto wa 2031.

Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye aliondoka kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar na tuzo ya mchezaji bora chipukizi, amekuwa na wakati mgumu kucheza mara kwa mara na kuhalalisha ada yake kubwa ya uhamisho.

Chelsea kwa ujumla wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwenye mbio za Ligi Kuu England.

Hata hivyo, wakala Uriel Perez, amekanusha kuwa kuna mipango yoyote ya kutafuta timu mpya.

“Mchezaji hana nia ya kuondoka,” alisema Perez aakiambia AS, akipinga moja kwa moja uvumi huo.

“Viongozi wa Chelsea walikuwa wazi sana na mradi huu. Ni mpango ambao ungekuwa mgumu mwanzoni kwa sababu wachezaji wapya na wachanga walikuwa wanakuja, lakini wakati vipande vya timu vinaungana vizuri. Chelsea walikuwa wanaendelea kusonga mbele.

“Tamaa ya Enzo Fernandez ni kuwa kwenye timu na kufanikiwa. Hatukutani na klabu yoyote au kujaribu kuzungumza na klabu yoyote. Tunajua nia ya mchezaji ni nini. Ni wazi, angependa klabu iwe katika nafasi nyingine,” alisema.

Ripoti ya Football Transfers iliyopata mvuto mkubwa kwenye mitandao ya kijami ilisema Perez atafungua mazungumzo na klabu mbalimbali kutafuta fursa nje ya Chelsea.

Fernandez hakuwa mchezaji mpya pekee aliyesaini mkataba mrefu isivyo kawaida baada ya kujiunga na The Blues.

Bila kutaja majina, gazeti la The Athletic limebainisha kuwa baadhi yao “wameonyesha masikitiko yao faragha” kwa kusaini mikataba mirefu.

Wachezaji 13 kwenye kikosi hicho wana mkataba hadi angalau mwaka 2030, huku Fernandez, Mykhailo Mudryk, Moises Caicedo na Nicolas JackSon wote wakiwa wamejifunga hadi mwaka 2031.

Kinara mfumo wa NeST aula, Mchengerwa atoa maagizo
Elimu magonjwa yasioambukiza inahitajika - Dkt. Mpango