Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa Wizara yake kuhakikisha kila kiongozi aliyekasimiwa Mamlaka katika eneo lake kuhakikisha anatumia mifumo inayotambuliwa na Serikali.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Februari 9, 2024 Jijini Dodoma wakati akimkabidhi zawadi ya Shilingi Milioni 10 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Happiness Msanga iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuwa taasisi ya umma iliyoongoza kitaifa katika kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST).
Waziri huyo wa TAMISEMI ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, ambayo awali ilieleza kuwa baada ya kutumia ipasavyo Mfumo wa NeST imeokoa kiasi cha Shilingi Milioni Nane kwa kila mwezi, zilizokuwa zinatumika kwenye ununuzi wa bidhaa. Hivyo, Halmashauri hiyo inaokoa takriani Sh. 96 Milioni kwa mwaka kwa ununuzi wa bidhaa pekee.
Aliongeza kuwa watendaji wa Serikali wanapaswa kuhakikisha wanatumia Mifumo ya TEHAMA kwakuwa huongeza uwazi, ushindani wa haki, uwajibikaji kuziba mianya ya rushwa na kusaidia wafikishia wananchi huduma kwa haraka na kwa wakati.
Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu wa TAMISEMI kuwaandikia barua watendaji wa halmashauri zote ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa NeST ili wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua kwa kutozingatia maelekezo ya Serikali.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu leo nisaini barua ya kuwapelekea watendaji wa Halmashauri ambazo hazitumii Mfumo wa NeST. Watueleze, kama ni suala la mafunzo PPRA wametueleza kuwa wako tayari kuwapa mafunzo tena bila malipo. Na kama ni suala la mtandao, tunaona hata Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imefanikiwa kutumia Mfumo, tuzielewe vipi zile ambazo ziko mjini na hazitumii?,” alisema Mchengerwa.
Vilevile, Waziri Mchengerwa aliwataka watendaji kuhakikisha wanatumia kikamilifu na bila kukwepa, mifumo yote iliyowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na Mfumo wa TAUSI, GOTHOMIS na mingine. Alionya kuwa wanaokwepa kutumia mifumo hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa (PPRA), Eliakim Maswi, alisema kuwa Mamlaka hiyo imeendelea kuzihimiza taasisi za umma kuhakikisha zinazingatia matakwa ya sheria na maelekezo ya Serikali, lakini bado zipo baadhi ya taasisi ambazo hazijaanza kutumia mfumo.
“Hadi leo, taasisi 1124 zimesajiliwa katika mfumo wa NeST. Kati ya Taasisi hizo, 998 zimesajili watumishi wake ambao kwa ujumla ni 33,749. Pia, taasisi 753 zimetangaza mipango yake ya ununuzi ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 yenye thamani ya shilingi Trilioni 28.6, na Halmashauri tatu hazijaanza kutumia mfumo,” amesema Maswi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Bi. Msanga aliishukuru Serikali kwa kuanzisha Mfumo wa NeST pamoja na zawadi iliyotolewa na PPRA kama motisha, akieleza pia sababu za kuibuka washindi wa kutumia Mfumo kuwa ni kuhakikisha watendaji wa Halmashauri hiyo wa kila idara wanapata elimu ya kutosha kuhusu Mfumo na kuhakikisha kila ununuzi unafanyika kwenye mfumo.
“Tulianza kupeana elimu na uelewa, tulianza kwa Wakuu wa Idara, Wakuu wa shule za msingi na Sekondari… na mwanzo tulienda kwa Mkuu wa Wilaya maana sisi Wilaya yetu tupo kijijini. Kwahiyo, wiki ya kwanza tukakubaliana kila ununuzi ufanyike kwenye mfumo, wiki ya pili na ya tatu tukajikuta tumeshazoea zaidi mpaka kufikia hapa tulipo,” alisema Bi. Msanga.