Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi ana mwaliko wa wazi wa kucheza katika kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki Michuano ya Olimpiki msimu huu wa majira ya joto, kwa mujibu wa kocha, Javier Mascherano.
Argentina waliwashinda washindi wa medali za dhahabu, Brazil kwa bao 1-0 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michezo ya Olimpiki huko Paris nchini Ufaransa baadae mwaka huu.
“Kila mtu tayari anajua uhusiano wangu na Leo Messi, urafiki nilionao,” amesema Mascherano.
“Milango ipo wazi kwa mchezaji kama yeye kuja kutusindikiza kwenye michuano ya Olimpiki, basi itategemea yeye na ahadi zake.”
Messi, ambaye aliiongoza nchi yake kunyakua taji lao la tatu la Kombe la Dunia mwaka 2022, alisherehekea Argentina kufuzu kwa Olimpiki kwa kutuma kwenye Instagram picha ya timu ya Mascherano.
Kiungo wa Argentina chini ya umri wa miaka 23, Thiago Almada alisema itakuwa na ndoto kuwa na mshindi wa Ballon d’or mara nane Messi kwenye kikosi cha Olimpiki.
“Natumani ana nia, kwamba anaweza kuwa huko,” alisema Almada anayeichezea Atlanta United.
“Lazima tuone jinsi alivyo wakati huo, itakUwa ndoto kwamba angeweza kucheza.”
Messi alishinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki mjini Beijing mwaka 2008 na rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach hivi majuzi alisema itakuwa “nzuri sana kwa michezo ya Olimpiki kumrejesha.”
Hata hivyo, Messi tayari ameeleza nia yake ya kutaka kushiriki michuano ya Copa America 2024 itakayoandaliwa nchini Marekani kuanzia Juni 20 hadi Julai 14, chini ya wiki mbili kabla ya michezo hiyo kuanza jijini Paris.