Kocha wa Walinda Lango wa Simba SC Daniel Cadena, amesema Benchi la Ufundi la timu hiyo linaamini Mshambuliaji wao mpya, Fredy Michael, ataanza kufunga mabao hivi karibuni pamoja na kwamba anakosa sana nafasi za wazi.
Mshambuliaji huyo Raia wa Ivory Coast alisajiliwa na Simba SC dirisha dogo akitokea Green Eagles ya Zambia na tayari amecheza mechi nne za timu hiyo dhidi ya Mashujaa, Tabora United, Azam FC na Geita Gold na kufunga bao moja.
Akizungumzia kiwango cha nyota huyo katika mechi hizo, Cadena amesema licha ya kuonekana kukosolewa pale anapokosa nafasi lakini benchi la ufundi linamuamini na litaendelea kumnsaidia kuzoea mazingira kwani ni sehemu ya mipango ya kikosi hicho katika mechi zijazo.
“Anaweza kuwa bado hajazoea mazingira na kuelewana na wachezaji wenzake lakini sisi tunamuamini kabisa kwenye mipango yetu na kocha (Abdelhack Benchikha) na sisi wasaidizi wake tutaendelea kumpa nafasi na kumsaidia katika mechi zijazo,” amesema Cadena.
Ameongeza mchezo uliopita dhidi ya Geita Gold, walipata ushindani mkubwa na walikabiliana na timu nzuri, huku akilia na ratiba kuwa inawabana na mazingira ya Uwanja wa CCM Kirumba kuwasumbua.
Tumeondoka na Pointi tatu lakini ilikuwa mechi ngumu kwetu kucheza katika uwanja huu na tulikuwa na ratiba ambayo tunapaswa kucheza mechi tano ndani ya siku 12, jambo ambalo ni gumu katika siku mbili tu maandalizi huwezi kufanya mazoezi ya kutosha na kurejesha miili vizuri, kwa hiyo ilikuwa ngumu kupata hizo Pointi tatu tulizozipata kwa hiyo tunapaswa kuendelea kupambana kila siku na kufanya vizuri.
“Sasa tunakwenda kwenye mipango ya michezo mingine minne kuhakikisha tunapata alama nyingi kama ilivyo malengo yetu, tutahakikisha msimu huu na sisi tunakuwa mabingwa,” amesema.