Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Fredy Felix Minziro ameahidi kuiondolea timu hiyo unyonge na kuirudisha kwenye ushindani kama ilivyokuwa zamani.
Akizungumza mjini Bukoba mkoani Kagera Minziro amesema, hiyo ni kutokana na wachezaji waliopo kuwa na uwezo mkubwa wa kushika haraka anachofundisha kwenye mazoezi.
“Nataka kuirudisha Kagera Sugar ya zamani ambayo iliogopwa hata na timu vigogo na hilo linawezekana kutokana na aina ya wachezaji niliokuwa nao kwenye kikosi changu, wana uwezo mkubwa wa kushika ninachowaelekeza,” amesema Minziro.
Amesema mechi mbili walizocheza katika uwanja wa nyumbani wa Kaitaba na kuvuna Pointi nne zimempa mwanzo mzuri wa kutimiza kile ambacho amekiahidi kwa uongozi na mashabiki wa timu hiyo.
Amesema kwa kuwa ameichukua timu hiyo ikiwa nafasi za chini kwenye msimamo, mikakati yake ni kuona wanashinda mechi zote watakazocheza nyumbani huku wakitafuta sare au ushindi katika mechi za ugenini.
Kagera Sugar chini ya Minziro juzi Jumatatu (Februari 12) ilipata ushindi wake wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Singida Fountain Gate na kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na Pointi 17.