Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Wilson Mahera amewataka waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi kuhakikisha wanawekeza katika mafunzo ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutoa huduma bora za afya kwa watanzania.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya Msingi, Dkt. Mahera amesema waganga wafawidhi wanapaswa kuwekeza katika mafunzo kwa ajili ya maendeleo ya kitaalamu.
Amesema, “Waganga wafawidhi wanapaswa kuwekeza katika mafunzo kwa ajili ya maendeleo ya kitaaluma ili kuhakikisha wanapata uelewa mpya na kuweza kwendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya afya, mkifanya hivyo kutawawezesha wanaweza kutoa huduma bora na hasa za kisasa kwa jamii ya kitanzania katika maeneo yenu.”
Aidha, ametoa wito kwa waganga wafawidhi hao kila mmoja wao kujitoa kikamilifu katika kutekeleza majukumu na kuwa karibu na jamii wanayoihudumia.