Serikali za nchi za Afrika Kusini, Nigeria na Ivory Coast zimewatunuku wachezaji wa timu zao za taifa za soka kwa kazi njema walizofanyia nchi hizo katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ iliyomalizika mwishoni mwa juma lililopita.
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara amempatia kila mchezaji wa kikosi cha ushindi cha Ivory Coast Dola za Marekani 82,000 (sawa na Sh milioni 207) na nyumba yenye thamani sawa na hiyo.
Pamoja na kupoteza kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali mbele ya Ivory Coast, Super Eagles ilipokewa nyumbani na Mamilioni ya Mashabiki na juhudi zao zilizawadiwa na Rais wa nchi hiyo, Bola Tinubu. Kila mtu katika kikosi cha Nigeria alipewa ardhi karibu na mji mkuu Abuja.
Timu ya Afrika Kusini iliyoshika nafasi ya tatu nayo ilitarajia kupata kiasi cha Dola za Marekani 52,000 (Sawa na Sh milioni 131) kwa kila mchezaji, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.