Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, Hanifa Suleiman amesema mvua zilizonyesha hivi karibuni ndio zimechelewesha kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa timu ya KMC FC.
Akizungumza jijini Dar es salaam Hanifa amesema licha ya changamoto hiyo wanatarajia kabla ya msimu huu kumalizika utakuwa umekamilika na kuchezwa michezo kadhaa.
Amesema kwa sasa uwanja huo ambao una uwezo wa kuingiza mashabiki 5,000 imebaki kukamilisha eneo la kuchezea ili kutandika zulia.
Kuhusu kutumika kwa mechi zinazohusu Simba SC na Young Africans dhidi ya KMC amesema wangependa zichezwe hapo ila kutokana na uwanja kubeba mashabiki wachache wataangalia wacheze wapi ili kukidhi mahitaji ya mashabiki na usalama pia.
Ujenzi wa uwanja huo unaojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ulianza mwaka 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 2.7.
KMC pia ilinunua basi jipya na la kisasa kwa ushirikiano na benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kuwa miongoni mwa klabu zenye mabasi bora kabisa nchini.