Kocha Mkuu wa Simba SC Benchikha amesema anaendelea kukisuka kikosi chake kulingana na aina ya mpira anaocheza mpinzani wao Asec Mimosas, na kwamba kikubwa anahitaji ushindi katika mchezo huo.

Simba SC itakuwa mgeni wa Asec Mimosas Jumamosi (Februari 24), katika mchezo wa Mzunguuko wa tano wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Bounie mjini Abidjan.

Benchikha amesema kila eneo analifanyia kazi na kurejea kwa beki wake, Henock Inonga kikosi kimeongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi baada ya kukosekana kwenye michezo sita ambayo wameshacheza.

“Asec Mimosas tumekutana nao, tunawafahamu na wao wanatufahamu, tunaandaa mipango yetu ya kwenda kusaka matokeo chanya ugenini, tunaendelea kusahihisha makosa yetu tuliyoyaona katika mechi zilizopita,” amesema kocha huyo raia wa Algeria.

Simba SC chini ya Benchikha inaendelea kujiandaa na mchezo huo na habari njema ni kurejea kwa beki wao, Inonga ambaye alikuwa na timu yake ya Taifa, DR Congo iliyofanikiwa kumaliza nafasi ya nne katika michuano ya ‘AFCON 2023’.

Simba SC ilianza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Asec, ikasuluhu mbele ya Jwaneng Galaxy, ilifungwa 1-0 dhidi ya Wydad AC na kushinda 2-0 ilipopambana na Wydad.

Katika msimamno wa Kundi B, Simba SC ipo nafasi ya pili kwa pointi tano nyuma ya Asec yenye Pointi 10 kileleni, Jwaneng Galaxy ina pointi nne wakati Wydad ikiburuza mkia na alama tatu ambapo timu zote zimeshacheza mechi nne kila moja.

Uwanja KMC FC kukamilika Machi 30
Mmoja afariki kwa ajali ya Bajaji, Basi dogo Moro