Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, itacheza na Bulgaria kwenye mashindano maalumu yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka duniani ‘FIFA’ yajulikanayo kama ‘FIFA Series’, Machi 22, nchini Azerbaijan.
Mashindano hayo madogo yanayochukua nafasi ya mechi za kirafiki za kimataifa za FIFA yatashirikisha timu nne kutoka mabara ya Afrika, Ulaya na Asia.
Bara la Afrika litawakilishwa na Tanzania, Ulaya itawakilishwa na Bulgaria na Asia itawakilishwa na mwenyeji Azerbaijan na Mongolia.
Taifa Stars itacheza mchezo wake wa pili Machi 25 na timu ya Mongolia.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kukipiga Bulgaria na Mongolia katika michezo ya kirafiki iliyoandaliwa na FIFA mechi za kujipima ubavu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Clifford Ndimbo amethibitisha kuwepo kwa mashindano hayo na kusema Tanzania itashiriki na kwa sasa wako kwenye maandalizi ya awali kwa ajili ya michuano hiyo.
“Tuna taarifa ya kuwepo kwa haya mashindano ya ‘FIFA Series’ na sisi kama Tanzania tuko kwenye hatua za awali za kuona namna gani tunashiriki.
Tutayapa uzito unaostahili kwani tunaamini yataenda kuwa sehemu ya ujenzi mzuri wa timu yetu ya taifa kwa ajili ya mashindano mengine,” amesema Ndimbo.