Mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Luis Suarez amedai kwamba tukio lake la kumngata beki wa Italia Giorgio Chiellini lilisababisha Arsenal kushindwa kupata saini ya Mshambuliaji Karim Benzema.
Mwaka 2014, Suarez alikuwa tayari kuachana na Liverpool na klabu za Real Madrid na Barcelona zote zilionyesha dhamira ya kuhitaji huduma yake.
Real Madrid tayari ilikuwa imejiandaa kuachana na Benzema na nafasi yake kuchukuliwa na Suarez baada ya fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil.
Lakini, baada ya Mshambuliaji huyo kumng’ata Chiellini, alidai Real Madrid ilijitoa kwenye mbio za kumsajili. Na badala yake alikwenda kujiunga na Barca, hivyo Madrid ikambakiza Benzema na hapo Arsenal ikabaki mikono mitupu.
Suarez ameliambia La Mesa: “Kabla ya Kombe la Dunia 2014, Real Madrid ilitaka kunisajili na kila kitu kilikuwa vizuri. Walikuwa wanajiandaa kumuuza Benzema kwenda Arsenal, mambo yalishamalizwa.
“Kombe la Dunia lilipoanza, Barca ikaingia kwenye mbio na mimi chaguo langu lilikuwa Barca. Baada ya tukio la kumng’ata Chiellini, Madrid wakarudi nyuma na Barca wakaongeza juhudi. Mwisho wa yote nikachagua Barca, ambayo ilikuwa ndoto yangu.’
Tukio la Suarez kumng’ata Chiellini lilikuja mwaka mmoja baada ya kufanya kama hivyo kwa beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic. FIFA ilimfungia mechi tisa za kimataifa, lakini Barca ikamsajili.
Kwenye kikosi hicho cha Nou Camp, Suarez alishinda mataji manne ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Sasa Suarez ameungana na Messi, Inter Miami.